MAHAFALI URKI SEKONDARI TAREHE 17 OCTOBER 2015
Siku hii ilithibitisha ule usemi wa
Kiswahili kuwa siku njema huonekana asubuhi.
Wanafunzi wote walikua nadhifu na wenye haiba
ya kisomi wengi wao wakiwa wamevalia sare mpya huku nyuso zao zikiakisi mwanga
wa jua kwa tabasamu ambalo ni nadra sana kuliona shuleni na hasa shule za
Tanzania. Hili lilikuwa jibu tosha kwa wale waliokuwa wakiuliza shule hii ina
tofauti gani kubwa na shule nyingine? Mbona wazazi wengi wana watoto zaidi ya
mmoja katika shule hii?
Baada ya ibada iliyoongozwa na mchungaji
wa kituo (Chaplain) Mch Okuli Nkya, waafunzi na jumuiya nzima walikuwa na
mapumziko mafupi ya kunywa chai nzito kwa wote.
Mapumziko yalimalizika baada ya nusu saa
hivi na ndipo Maandamano ya kuingia ukumbinni yalipoanza kwa vishindo vya
kwaito la nguvu.
Ndani ya ukumbi kelele za shangwe
zilisikika kwa wale wanafunzi wangojezi ambao hawakuingia kwenye msafara huu,
kelele zao zilikuwa kama kelele za maji mengi mfano wa yale ya maanguko ya maji
ya Victoria kule Zimbabwe (Victoria Falls)
Mkuu wa shule Mwl Joseph Shahidi
alionekana mwenye furaha sana akitembea imara mithili ya askari tena wale
wa mkoloni KAR, huku mkononi akiwa amebeba simu yake Smart Phone na bahasha
yenye risala aliyomuandalia mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Hai.
Walimu na watumishi wengine nao walivalia
vizuri sana. Jikoni muda wote kulikuwa na pilika pilika za kuandaa mahanjumati
na kwa kuwa ukumbi haukua mbali sana na jikoni basi ungeweza kukisia aina za
vyakula vilivyokuwa vinaandaliwa na hata kiasi cha mishikaki iliyokuwa
imebanikwa jikoni.
Waandishi wa habari nao hawakuwa nyuma
kuchukua matukio. Kwa kweli siku hii ilionekana ya kipekeee sana na yenye
baraka zake nyingi sana.
Chapisho linalofuata litaelezea
kinagaubaga ratiba nzima ya siku hiyo na tathmini ya wageni waliohudhuria. Hapa
utweza kuona pia video na picha mnato nyingi kadri inavyowezeka.
Aidha kiamabatanisho cha risala zote na
hotuba zote zilizotolewa siku hiyo zitajumuishwa.
Utapata nafasi ya kuwaona wahitimu wote na
walimu baadhi waliokuwepo
Kwa sasa tuishie hapa